Pages

Ads 468x60px

.

About

.

Monday, July 2, 2012


HOTUBA YA RAIS KIKWETE

ASIE KUBALI MSHAHARA WA SERIKALI AFUNGE VIRAGO



WAKATI Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk Steven Ulimboka akiendelea na matibabu Afrika Kusini, Rais Jakaya Kikwete amesema Serikali haihusiki na kilichomtokea daktari huyo kwa kuwa alikuwa kiungo muhimu katika majadiliano baina ya pande hizo mbili.


Rais Kikwete alisema hayo jana katika hotuba yake ya kila mwezi, ambapo mbali na suala hilo, pia alizungumzia sababu za mgomo wa madaktari na usafirishaji wa wahamiaji haramu.


Dk Ulimboka ambaye alikuwa anaratibu mgomo wa madaktari unaoendelea nchi nzima kutokana na Serikali kushindwa kutimiza madai yao mbalimbali, anatibiwa figo na majereha aliyoyapata katika sehemu mbalimbali za mwili, baada ya kutekwa na watu wasiojulikana, kisha kupigwa, kung'olewa kucha, meno mawili na kutupwa katika Msitu wa Pande, usiku wa kuamkia Jumatano iliyopita.
Tangu kutokea kwa unyama huo uliofanywa na watu wasiojulikana, baadhi ya wananchi na wanaharakati wamekuwa wakiilaumu Serikali kuwa inahusika na utekaji huo na wengine wakienda mbali zaidi, kuwa watekaji walikuwa wanamlazimisha kueleza nani yuko nyuma ya mgomo wa madaktari. 
Rais Kikwete, kama awali alivyosema Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, walisema wanatambua kuwa, Serikali nayo inatajwa katika orodha ya wanaotiliwa shaka kuhusu kilichomtokea Dk Ulimboka, lakini yeye ameshangazwa na hisia hizo, kwani haoni sababu ya Serikali kufanya hivyo.


"Dk Ulimboka alikuwa kiungo muhimu katika mazungumzo baina ya Serikali na madaktari. Ni kweli kwamba yeye si mtumishi wa Serikali, hivyo hakustahili kuwa sehemu ya majadiliano haya.  Kulikuwa na rai ya kutaka asiwepo, lakini nilisema wamuache maadam madaktari wanamwamini kuwa anaweza kuwasemea vizuri zaidi kuliko wao wenyewe walioajiriwa na Serikali," alisema Rais Kikwete.
Alisema Serikali haina sababu ya kumdhuru Dk Ulimboka kwa sababu suala la mgomo, Mahakama Kuu imekwishatoa amri ya kuusitisha, hivyo anayekaidi amri hiyo atakuwa ananunua ugomvi na mhimili huo wa dola, ambao wenyewe una mamlaka ya kumtia adabu.
"Hivi baada ya kufika hapo Serikali iwe na ugomvi na Dk Steven Ulimboka kwa sababu ipi na jambo lipi hata iamue kumdhuru?" alihoji na kuongeza:
"Kama kuna mtu wa Serikali kafanya, itakuwa kwa sababu zake binafsi na siyo za Serikali au kwa kutumwa na Serikali," alisema Rais Kikwete.


Alisema alichofanyiwa Dk Ulimboka kimemsikitisha na kumhuzunisha kwa kuwa ni kitendo cha kinyama na kinyume kabisa na mila na desturi za Tanzania.
Alisema Watanzania hawajazoea mambo hayo na kwamba ameelekeza vyombo vya ulinzi na usalama kufanya uchunguzi wa kina ili ukweli ujulikane.  
"Nimesema kuwa ningependa ukweli huo ujulikane mapema ili tuondoe wingu baya la kutiliana shaka na kulaumiana kunakoendelea hivi sasa," alisema.
Alisema anatoa mkono wa pole kwa Dk Ulimboka na kumwombea apone haraka ili aungane na familia yake na Watanzania wenzake katika ujenzi wa taifa. 
Rais Kikwete pia alimpongeza Juma Mgaza ambaye alimsaidia Dk Ulimboka kumtoa katika pori alikotupwa na kumpeleka kituo cha polisi kwa moyo wake wa huruma.


KUHUSU MGOMO
Kuhusu mgomo unaoendelea Rais Kikwete alisema, kiwango cha mshahara cha Sh3.5 milioni wanachokitaka madaktari Serikali haina uwezo wa kukitoa, hivyo daktari anayeona kuwa hawezi kufanya kazi serikalini bila ya kulipwa mshahara huo, awe huru kuacha kazi na kwenda kwa mwajiri anayeweza kumlipa kiasi hicho.
Rais Kikwete alisema, kwa sasa Serikali haiwezi kuwaahidi kuwa inao uwezo wa kuwalipa mshahara wa kuanzia wa Sh3.5 milioni na posho zote zile, kwani ikifanya hivyo malipo ya daktari anayeanza kazi yatakuwa Sh7.7 milioni kwa mwezi, kitu ambacho haitakiweza. 
"Si vyema kutoa ahadi hewa kwa watu tunaowaheshimu na kuwathamini kama walivyo madaktari. Kutokana na ukweli huo basi kama daktari anayeona kuwa hawezi kufanya kazi serikalini bila ya kulipwa mshahara huo awe huru kuacha. Nasi tutamtakia kila la heri,"alisema Rais Kikwete.


Rais Kikwete alisema, madaktari hawana sababu ya kugoma ili washinikize kulipwa mshahara huo kwani uwezo haupo.
"Kwa nini upate usumbufu wa kuachishwa kazi na kutakiwa kuondoka kwenye nyumba ya Serikali ndani ya saa 24. Jiepushe na yote hayo kwa kujiondoa mwenyewe," alisema.
Alisema mamlaka za ajira zimeanza kuchukua hatua hizo kwa wale wanaokwenda kinyume na sheria za kazi na wataendelea kufanya hivyo kwa wote wanaoendelea kugoma.  
Alisema anajua baada ya hatua hizo kuchukuliwa kuna manun’guniko ya kuonewa yatajitokeza, lakini ni bora kufanya hivyo ili ijulikane Serikali haina daktari. 


"Mlitegemea mwajiri afanyeje? Ni bora kufanya hivyo ili ajue hana daktari aweze kufanya utaratibu wa kuziba hilo pengo na huyo anayekuja awe na mahali pa kuishi."
Kutokana na hali hiyo amewasihi madaktari kuacha mgomo na kurejea kazini, kwani Watanzania wanateseka na kupoteza maisha. 


SABABU YA MGOMO
Rais Kikwete alisema kwamba, kuna masuala matatu ambayo yamekuwa na mwafaka kwa kiasi fulani na kutoafikiana kwa baadhi ya mambo kati ya madaktari na Serikali.
Alisema suala la kwanza ni suala la kufanya kazi katika mazingira hatarishi ambalo Serikali imekubali hoja ya kuchukua hatua ya kuwalinda madaktari wanaofanya kazi katika mazingira hatarishi. 


Pia alisema Serikali imeeleza dhamira ya kurudisha posho ya mazingira hatarishi kwa watumishi wa umma wanaostahili na utekelezaji wake utafanyika baada ya uchambuzi wa kina wa kubainisha mazingira hatarishi ni yapi, viwango stahiki viwe vipi na nani hasa wahusike. 
Rais Kikwete alisema kuwa, madaktari wamekataa suala hilo la kufanya uchambuzi, wanataka kiwango kiwe kama wanavyotaka wao, yaani asilimia 30 ya mshahara na kianze mara moja.


Alisema suala la pili ambalo wamekubaliana nusu nusu ni kuhusu nyumba za kuishi ambalo Serikali imekiri wajibu wake wa kuwapatia nyumba za kuishi.  
Rais Kikwete aliongeza kwamba, kwa maeneo ambayo madaktari wanalipwa posho ya pango, Serikali imesema waajiri wataendelea kufanya hivyo kwa mujibu wa taratibu zilizopo kwa watumishi wa umma wenye stahili ya kupewa nyumba.


Alisema jambo hilo limekataliwa na madaktari na kutaka lazima walipwe asilimia 30 ya mshahara kama posho ya nyumba. 
Rais Kikwete alisisitiza kwamba, Serikali kwa upande wake imeona vigumu kufanya hivyo na kuwasihi wakubali wanayotendewa kama wafanyakazi wengine wote wa umma.


Alisema suala lingine ambalo lilikuwa na makubaliano ya nusu nusu ni kuhusu posho ya kufanya kazi katika mazingira magumu na pande zote mbili ziliafikiana kuwa yapo baadhi ya maeneo nchini yanayo mazingira magumu kwa watumishi wa umma, hivyo hatua zichukuliwe kuwasaidia watumishi hao. 
Kuhusu posho, alisema Serikali imekubali kuwapo posho ya aina hiyo ila itatekelezwa baada ya kufanya uchambuzi wa kuainisha mazingira husika, kutambua watumishi waliopo na gharama zake.
Alisema madaktari hawajakubali kusubiri zoezi la uchambuzi lifanyike, wanataka Serikali ilipe posho hiyo sasa.  


"Tofauti hapa si posho hiyo kuwapo, bali ni rai ya Serikali ya kubaini maeneo yenyewe na kupanga aina ya hatua na viwango vya posho kulingana na mazingira halisi ya maeneo. Madaktari hawaoni haja ya kufanya hayo," alisema.
Alisema kuna mambo mawili ambayo hayakuwa na mwafaka kabisa kati ya pande hizo mbili na la kwanza ni posho ya kuitwa kazini (on call allowance). 
Rais Kikwete alisema, Serikali ilishaongeza posho hizo tangu Februari, 2012 posho iliongezwa kutoka Sh10,000 hadi Sh25,000 kwa daktari bingwa, Sh20,000 kwa dakari mwenye usajili wa kudumu na Sh15,000 kwa madaktari waliohitimu ambao wapo katika kipindi cha mafunzo kazini (Interns). 
Alisema hata hivyo, madaktari kwa upande wao hawakukubali uamuzi huo wa Serikali na kusisitiza walipwe asilimia 10 ya mshahara. 


Rais Kikwete alisema ugumu wa kukubali pendekezo la madakari ni kuwa sharti la malipo haya ni mtu kuitwa kazini na kwamba ukitaka ilipwe kiwango cha mshahara ina maana kuwa hata kama daktari hakupangwa kuitwa au alipangwa na hakutokea aendelee kulipwa.
 Alisema jambo la pili ambalo mwafaka haukufikiwa baina ya Serikali na madaktari ni kuhusu mshahara wa kuanzia kazi wa daktari ambao madaktari wanataka uwe Sh3.5 milioni wakati Serikali inasema kiasi hicho hatukiwezi.
Alisema Serikali imeeleza utayari wake wa kuongeza mshahara kwa kati ya asilimia 15 mpaka 20 kama ambavyo itafanya kwa watumishi wote wa umma katika mwaka huu wa fedha.  
Rais Kikwete alisema, kwa kiwango cha sasa cha mshahara wao, daktari ataanzia kati ya Sh1.1 milioni na Sh1.2 milioni kutegemea kiwango kipi hatimaye kitaamuliwa.
"Madaktari wamekataa katakata na wameng’ang’ania Sh3.5 milioni," alisema.


Alisema ni muhimu madaktari wakatambua kuwa wagonjwa wanateseka na wengine kupoteza maisha kwa mgomo usiokuwa halali kisheria ambao pia haustahili kuwapo hata kwa mujibu wa maadili ya udaktari.
Alisema viongozi wa MAT na wenzao wanawaingiza madaktari katika mgogoro na mahakama na waajiri wao isivyostahili.  
Rais Kikwete alisema ni vyema viongozi wa madaktari na madaktari wakatambua kuwa wanashiriki katika mgomo usiokuwa halali ambao pia kiongozi wao mkuu amekana mahakamani kuwa hahusiki nao. 


Rais Kikwete alisema madaktari lazima watambue pia kwamba ajira zao wanaziweka hatarini kwani mfanyakazi hana kinga ya kutofukuzwa kazi na mwajiri kwa kushiriki mgomo unaokubalika kisheria. 
"Huu siyo. Watapoteza ajira, hawana pa kukimbilia, hawana cha kuwalinda. Kwa madaktari interns, wanahatarisha maisha yao, kwani hawatapata cheti cha kudumu wakishiriki mgomo usiokuwa halali. Lazima watafakari kwa hayo wafanyayo," alisema. 


Saturday, June 23, 2012

DOWNLOAD 2012/13 BUDGET

CLICK HERE TO DOWNLOAD














ALIPUA UFISADI NA MGODI ULIVYOUZWA

SAKATA la ufisadi katika uuzwaji wa mgodi wa makaa ya mawe wa Kiwira, mkoani Mbeya limeibuka upya, safari hii ikielezwa na Mbunge wa Musoma Vijijini (CCM), Nimrod Mkono kuwa umeuzwa kwa bei ya kutupa.Mbunge huyo ambaye ni mwanasheria, amelitaka Bunge kuunda Kamati Teule kwenda kuchunguza ufisadi huo, huku akihoji sababu za Serikali kuutengea mabilioni ya shilingi wakati umekwishauzwa.

Mkono alisema kuwa, “Mgodi huo wenye thamani ya matrilioni ya shilingi, umeuzwa kwa bei ya kutupa ya dola 700,000 tu za Marekani (Sh1.1 bilioni), kwa kampuni ya Intra Energy ya Australia.”

Mgodi wa Kiwira uliwahi kuzua malalamiko baada ya kumilikishwa kwa Kampuni ya ANBEN Limited, mali ya Rais Mstaafu Benjamin Mkapa na mkewe, Anna Mkapa, lakini Januari mwaka huu, aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja aliieleza Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), kuwa ANBEN Limited haihusiki tena na mgodi huo.

Alifafanua kuwa kampuni hiyo iliondolewa kuwa miongoni mwa wamiliki wa hisa kwa vile haikuweza kulipia hisa 200,000 ilizokuwa imechukua wakati wa usajili wa Kampuni ya Tan-Power Resources (TPR).

Akichangia mjadala wa Bajeti jana, Mkono alihoji sababu za Serikali kutenga Sh40 bilioni kwa ajili ya kulipa watu wa mgodi wa Kiwira ilhali inajua kuwa mgodi huo uliuzwa kwa bei ya kutupwa tangu mwaka 2007.

“Tumetenga Sh40 bilioni za kuwalipa watu waliotuibia fedha zetu, eti tunasema kwamba tunalipa madeni, haya ni madeni gani ambayo tunakwenda kulipa huko?” alihoji Mkono.

Alisema mwaka 2007 wabunge walipiga kelele wakiitaka Kampuni ya Tan Power iliyokuwa mbia wa Serikali katika mgodi huo, kuurudisha serikalini, lakini mwaka jana kampuni hiyo iliuza mgodi huo kwa bei ya kutupa.

“Unauzaje mgodi huu wenye thamani ya matrilioni ya pesa kwa bei hii ya kutupa?” alihoji na kuendelea, "Haya ni mambo ya ajabu sana. Tungeweza kupata fedha nyingi sana kutokana na mgodi huu na fedha hizi zingetusadia katika kugharimia mahitaji yetu ya bajeti.”

Mbunge huyo aliungana na wabunge wengine kuiponda Bajeti ya Serikali kwa kutegemea fedha za wahisani, huku rasilimali za nchi zikiendelea kufujwa bila huruma.

Alisema nakisi inayoonekana kwenye Bajeti, inatokana na uwezo mdogo wa kukusanya fedha za ndani licha ya kwamba nchi ina utajiri mkubwa wa madini, ambayo hata hivyo, yanawanufaisha watu wengine na kuwaacha Watanzania wakitaabika.

Mkono pia aliishambulia Serikali kwamba ‘ilichakachua’ mradi wa uchimbaji wa madini katika mgodi wa Buhemba na kuwadanganya wananchi ambao hawakunufaika na kitu chochote.

Kutokana na hilo, mbunge huyo alisema kuwa Bajeti ya mwaka 2012/13 imetoa upendeleo kwa baadhi ya maeneo huku ikiyaacha mengine muhimu, ambayo yanagusa masilahi ya wananchi.

“Serikali ilichakachua Buhemba lakini inapeleka tena Sh1 bilioni huko na sijui zinakwenda kufanya nini wakati ingeweza kupeleka katika moja ya shule za jimboni kwangu, au hata kama ingetusaidia wananchi wa Mara kujenga chuo kikuu cha kilimo ambacho kinajengwa mkoani kwetu,’’alisema Mkono.

Alisema yeye binafsi haelewi Serikali inaposema haina fedha kwani migodi ya Kiwira na Buhemba ingetumika vizuri, ingeweza kuipatia Serikali kiasi kikubwa cha fedha kinacholingana na fedha zinazotolewa na wafadhili. 

Friday, June 22, 2012


MGOMO WA MADAKTARI KUANZA LEO

JUMUIYA ya Madaktari imetangaza rasmi kuanza kwa mgomo usio na kikomo kuanzia leo, huku ikidai Serikali imekataa kutekeleza madai yao yote yaliyowasilishwa katika kamati ya majadiliano iliyoundwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.Wakati madaktari hao wakitangaza kurejea rasmi katika mgomo huo uliositishwa miezi mitatu iliyopita, Pinda aliliambia Bunge jana wakati akijibu Maswali ya Papo kwa Papo, kuwa mgomo huo ni batili na haukubaliki.


Saa chache baada ya Pinda kutoa onyo hilo lililorushwa moja kwa moja na vituo vya televisheni na redio kutoka Dodoma, madaktari hao wakiwa jijini Dares Salaam walitangaza mgomo huo wenye lengo la kushinikiza Serikali kutekeleza madai yao.


Mgomo huo ulitangazwa kwa waandishi wa habari na Dk Stephen Ulimboka, muda mfupi baada ya kukamilika kwa mkutano wa ndani wa madaktari, uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jengo la Utamaduni la Watu wa Urusi.


Dk Ulimboka alisema mgomo huo usio na kikomo utawahusu madaktari wa kada zote nchini, na unatarajiwa kuanza kesho, baada ya wiki mbili walizotoa kwa Serikali kumalizika bila ya makubaliano yoyote.

“Madaktari kwa ujumla wao wamekubaliana kuwa watarejea katika mgomo usio na kikomo, hii ni kutokana na kugundua kuwa hakuna dhamira ya dhati ya Serikali, kumaliza mgogoro kati yetu na Serikali, uliodumu kwa muda mrefu sasa,” alisema Dk Ulimboka na kuongeza,

Thursday, June 21, 2012


UOZO WA TBS KUANZA KUISHA

SIKU chache baada ya Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Abdallah Kigoda kuiagiza Bodi ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kumsimamisha kazi Mkurugenzi wake Charles Ekelege, shirika hilo limetangaza kampuni zilizopewa kazi ya kukagua magari yanayotoka nje ya nchi.

Mapema mwezi uliopita Dk Kigoda alitoa agizo hilo la kumsimamisha kazi Ekerege ili kupisha taratibu za kisheria ikiwamo uchunguzi kufanyika dhidi yake kutokana na madai ya TBS kuwa na ofisi hewa za ukaguzi wa magari nje ya nchi. 

Sakata la Ekelege liliibuliwa mwanzoni mwa mwaka huu,  ambapo Kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma (POAC), chini ya Makamu Mwenyekiti wake, Deo Filikunjombe ilimtuhumu mkurugenzi huyo baada ya  kubaini kuwepo kwa udanganyifu kwenye mpango wa TBS wa kukagua bidhaa nje ya nchi.  Filikunjombe alieleza kuwa waligundua madudu baada ya kutembelea vituo vya ukaguzi wa magari nchini Singapore na mjini Hong Kong, China ambapo walikuta vituo hewa vya ukaguzi wa magari.

Lakini jana, shirika hilo  lilitoa tangazo lililotolewa na Kaimu Mkurugenzi wake mkuu, linataja kampuni zilizopewa na zilizopokonywa kazi ya kukagua magari.

Tangazo hilo limeeleza kuwa tangu Juni 18 mwaka huu TBS imefuta leseni Na 0656 ya ukaguzi wa magari iliyokuwa ikifanywa na gereji ya  Jaffar Mohammed Ali iliyopo Dubai ambayo ilikuwa ikikagua magari yanayoingizwa nchini kutoka nchi hiyo.

“Kutokana na tangazo hili wote wanaoingiza magari kutoka Dubai wanashauriwa kupeleka magari yao kukaguliwa na kampuni ya Jabal Kilimanjaro Auto Elect Mechanical, magari ambayo yataingizwa nchini bila kukaguliwa na kampuni hii hayataruhusiwa kuingizwa katika soko la Tanzania,” lilieleza tangazo hilo.

Pia, lilieleza kuwa limefuta leseni Na 0655 ya kampuni ya WTM Utility Services ya nchini Uingereza kujihusisha na ukaguzi wa magari na badala yake magari yote kutoka nchini humo yanatakiwa kukaguliwa na kampuni ya Vehicle Operator Services Agency (VOSA).

“Magari yatakayoingizwa nchini kutokea Uingereza bila kukaguliwa na kampuni hii ya VOSA  hayataruhusiwa kuingia katika soko la Tanzania” lilieleza tangazo hilo.



MTEI AMTETEA JOHN MNYIKA

MWASISI wa Chadema, Edwin Mtei amemtetea Mbunge wa Ubungo, John Myika kuwa alikuwa sahihi kusema kwa Rais Jakaya Kikwete ni dhaifu, kwa kuwa kuna matukio mengi yaliyohitaji uamuzi wake na hakuutoa kwa wakati.

Pia Mtei amelaumu Kanuni za Bunge zilizomwezesha Naibu Spika, Job Ndugai kumtoa nje ya ukumbi wa Bunge mbunge huyo.

  Juzi, Mnyika alitolewa nje ya ukumbi wa Bunge, baada ya kukukataa kufuta kauli yake kuwa ‘Rais Jakaya Kikwete ni dhaifu’.
Akitetea kauli hiyo, Mtei alirejea baadhi ya matukio aliyodai yanaonyesha udhaifu huo, ukiwamo uamuzi ya Rais Kikwete juu ya hatua za kuwachukulia walioiba fedha katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Mtei alifafanua kwamba,  kitendo cha Rais  Kikwete kuwataka wezi hao warudishe fedha walizoiba badala ya kuwakamata, kinadhihirisha udhaifu mkubwa wa kiongozi huyo.

  “Rais Kikwete ana udhaifu wa kuwachukulia hatua za kisheria watu ambao wanahujumu taifa  kwa ufisadi…udhaifu wa Rais ni kama kutowadhibiti wezi wa fedha zetu kama fedha za EPA. Aliwaambia wezi warudishe fedha, badala ya kuwatia ndani wanabaki wanatamba kwa kuiba fedha zetu,” alisisitiza Mtei aliyewahi kuwa Gavana wa Benki Kuu.

 Alisema kibaya zaidi ni kwamba, nchi inayumba kutokana na uongozi mbovu kuanzia ngazi ya urais hadi chini, kwa kuwa tunaongozwa na watu wasiojua na kuisimamia Katiba.

Akitoa maoni yake juu ya Bajeti ya Serikali ya mwaka huu, Mtei alisema Bajeti hiyo haina jipya kwa kuwa haishughulikii matatizo na kero za wananchi.

Alisema Bajeti hiyo ambayo mjadala wake unahitimishwa kesho, haiwezi kukabilina na mfumuko wa bei unaolikabili taifa.

Kuhusu suala la deni la Taifa linalofikia Sh20.2 trilioni, alisema nchi ipo njia panda, hali ambayo ni hatari kwa kuwa ni mzigo kwa taifa na linazidi kuongezeka kila mwaka.

Mwanasiasa huyo ambaye ni Mwenyekiti wa kwanza wa Chadema, aliponda vitendo vya Serikali kukopa fedha kila mara kwenye mabenki ya kibiashara nchini, na kuomba kwa wahisani.



 
 
Animated Social Gadget - Blogger And Wordpress Tips